Utangulizi:
TAWASANET imesikitishwa na taarifa ya janga la mafuriko ya maji iliyoambatana na maporomoko ya udongo katika Mkoa wa Manyara, janga ambalo limeathiri taswira ya maisha ya baadhi ya wakazi wa eneo la Katesh, kukatisha uhai kwa baadhi ya wananchi, na kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya Maji na Usafi wa Mazingira.
TAWASANET inatambua kwamba janga la mafuriko na madhara yake limerudisha nyuma juhudi za Serikali na Wadau mbalimbali wa Maendeleo katika kuhakikisha upatikanaji wa Maji Safi na Salama kwa wakazi wa eneo husika, pamoja na huduma za Usafi wa Mazingira.
TAWASANET inatambua pia kwamba uharibifu wa miundombinu unaongeza hatari ya kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na homa ya matumbo, yanayohusiana na kuchanganyika kwa Maji safi na Maji taka, hivyo kuhitaji hatua za ziada kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Utambuzi wa Juhudi zinazoendelea
TAWASANET inatambua na kupongeza juhudi kubwa na za haraka zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na:
- Serikali katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kutuliza taharuki kubwa iliyosababishwa na janga hili na mipango ya huduma za dharura iliyowekwa.
- Vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama kwa kuchukua hatua za haraka za uokoaji wa wahanga na waathirika wa janga hili.
- Wadau wengine wa Maendeleo hususani Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Sekta Binafsi kwa kutoa michango ya hali na mali ili kupunguza madhila ya janga hili.
Kwa pamoja, tunaamini tutaleta nafuu ya mapema kwa waathiriwa wote.
Wito
Ili kuhakikisha ushirikiano unadumishwa katika kipindi hiki kigumu, na huduma zinaendelea kuwafikia wahanga na waathirika, TAWASANET inatoa wito na mapendekezo yafuatayo;
- TAWASANET inashauri juhudi hizi ziendelee kuratibiwa vizuri katika kuongeza tija, na hatimaye kurejesha hali ya kawaida kwa wakazi wa eneo lililo athirika.
- Kufanya tathmini ya mapema kutambua mahitaji halisi ya waathirika ili kurahisisha taarifa kwa Wadau wa Maendeleo wakiwemo Asasi za Kiraia kuhusiana na mahitaji (ya muda mfupi, wa kati, na muda mrefu). Hili litarahisisha ufanyaji maamuzi kwa Wadau wa Maendeleo wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na janga hili.
- Kuandaa taarifa ya kina itakayosaidia kuboresha mifumo ya ufuatiliaji, utambuzi wa mapema na kukabiliana na majanga (katika upande wa Sera, na uhalisia katika utekelezaji). Hii itasaidia namna ya kukabiliana na majanga kwa siku zijazo, endapo yatatokea ili kupunguza au kuzuia kabisa madhara kwa wananchi
Nafasi ya Asasi za Kisekta
TAWASANET inaendelea na juhudi ya kuhamasisha Asasi za Kisekta na Wadau wa Maendeleo kwa ajili ya:
- Kukusanya na kufikisha (kwa kadiri inavyowezekana), mahitaji muhimu kwa wahanga na waathirika.
- Kufanya tathmini na kuishauri Serikali namna bora zaidi ya kukabiliana na majanga (kabla, wakati, na baada).
- Kutoa wito kwa Wadau wa Maendeleo, kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zilizopo, kufanikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa wahanga na waathirika.
Hitimisho
Sote tuna jukumu mahususi la kufanya katika kipindi hiki cha janga lililotokea. Kama wadau muhimu, tuunganishe juhudi ili kuhakikisha wahanga na waathirika wa janga hili wanapata huduma muhimu, ikiwemo Maji Safi na Salama, Usafi wa Mazingira, na tiba.
Tunawaombea afya njema majeruhi wote, na faraja ya Mwenyezi Mungu wale wote waliopoteza wapendwa wao wa karibu ili warejee katika hali zao na mazingira yao ya awali mapema, hatimaye kuendelea na majukumu ya kujenga Taifa letu.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika Tuunganishe nguvu zetu na kushikamana Asanteni
Imetolewa na:
Mhandisi Herbert Kashililah
Mwenyekiti wa Bodi ya TAWASANET
5 Disemba 2023